Vyakula 5 Vinavyoongeza Maziwa Kwa Mama Anayenyonyesha.

Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.

Leo tujifunze baadhi ya vyakula vinavyosaidia kuongeza maziwa kwa mama anayenyonyesha. Ungana nami katika somo hili.

Mama anayenyonyesha anahitaji lishe bora ili kuongeza uzalishaji wa maziwa na kuhakikisha afya njema kwa mtoto wake.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Chakula na Lishe Nchini Tanzania (TFNC) asilimia 98 ya wanawake huwanyonyesha watoto wao na asilimia 58 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo (exclusive breast feeding). 

Pamoja na asilimia 98 ya wanawake kuchagua kuwanyonyesha watoto bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowafanya kushindwa kutekeleza kwa usahihi zoezi la unyonyeshaji ikiwemo mama kukosa maziwa ya kutosha.

TFNC wanabainisha kuwa mama anayenyonyesha anatakiwa kula lishe bora kutokana na kuwa na mahitaji makubwa ya virutubisho mwilini kwa ajili ya afya yake na kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mtoto.

Njia mojawapo ya mama kuzalisha maziwa ya kutosha ni kupitia kula vyakula vyenye lishe katika milo mitatu kamili ya kila siku pamoja na asusa.

Asusa ni kiasi kidogo cha chakula ambacho si mlo kamili, kinachoweza kuliwa bila matayarisho makubwa na huliwa kati ya mlo mmoja hadi mwingine.

Kwa mujibu wa TFNC, mama anayenyonyesha anashauriwa kuchagua asusa  zenye virutubisho muhimu kama  matunda, vyakula vilivyochemshwa au kuchomwa na kuepuka asusa zilizokaangwa, zenye sukari au chumvi nyingi.

Vifuatavyo ni baadhi ya vyakula vinavyosaidia kuongeza maziwa kwa mama anayenyonyesha ambavyo ni pamoja na:

1) Nafaka Nzima.

Uji wa nafaka kama vile uji wa mtama, mahindi, au ulezi ni maarufu katika jamii nyingi kwa ajili ya kuongeza maziwa. Nafaka hizi zina wingi wa virutubisho na madini yanayosaidia uzalishaji wa maziwa.

Kumbuka:

Vyakula vinavyotokana na nafaka isiyokobolewa kama vile ulezi, mtama, mchele wa ‘brown’  vinashauriwa zaidi kwa mama anayenyonyesha kwani vinaathari kidogo katika kiwango cha sukari mwilini na utengenezaji wa insulini kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka iliyokobolewa.

2) Maji.

Maji ni muhimu katika kuongeza kiwango cha maziwa ya mama anayenyonyesha kwani yanahusika pakubwa katika utengenezaji wa maziwa. TFNC  wanashauri mama anayenyonyesha atumie angalau bilauri nane za maji kwa siku au lita moja na nusu.

Kwa mujibu wa mtandao wa elimu ya malezi wa Africaparent mama anayenyonyesha anapaswa kuepuka vinywaji vilivyoongezwa sukari au kafeini na kutumia kwa wingi vimiminika kama vile supu au juisi za matunda.

3) Mboga Za Majani.

Mboga za kijani kama spinach, sukuma wiki, mchicha, na brokoli zina madini ya chuma na kalsiamu ambayo ni muhimu kwa mama anayenyonyesha.

4) Matunda.

Matunda kama vile mapapai, parachichi, ndizi, na machungwa yana vitamini na madini muhimu kwa afya ya mama na uzalishaji wa maziwa.

5) Vyakula Vya Protini. 

Vyakula vyenye protini kama vile nyama nyekundu, samaki, mayai, maziwa na bidhaa za maziwa, maharage na jamii zake, ni sehemu muhimu ya lishe kwa mama anayenyonyesha kwa sababu vinahitajika kwa ajili ya ukuaji na maendeleo ya mtoto, pamoja na kusaidia mama kupona na kudumisha afya yake baada ya kujifungua.

Mama anayenyonyesha anahitaji kiwango cha ziada cha protini kila siku ili kuzalisha maziwa ya kutosha kwa mtoto.

HITIMISHO:

Maziwa ya mama ni chakula muhimu na cha msingi kabisa kwa watoto waliopo kwenye umri wa kunyonya. Wataalamu wa afya wanashauri mtoto apewe maziwa ya mama peke yake kwa muda wa miezi sita ndipo aanze kupewa vyakula vingine laini.