- Dr. ISAYA FEBU Newsletter
- Posts
- Vyakula Hatari Kwa Mama Mjamzito.
Vyakula Hatari Kwa Mama Mjamzito.
Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.
Leo tujifunze kuhusu vyakula kadhaa ambavyo mama mjamzito anapaswa kuepuka au kula kwa tahadhari ili kulinda afya yake na mtoto aliye tumboni. Ungana nami katika somo hili.
Lishe bora ni muhimu sana kwa mama mjamzito ili kuhakikisha afya yake na ya mtoto anayekua tumboni.
Ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema pamoja na akili timamu, akiwa tumboni lazima alishwe lishe bora na mlo sahihi. Mwenye jukumu la kutoa lishe bora na sahihi kwa kiumbe kilichomo tumboni ni mama.
Hata hivyo, wakati wa ujauzito kuna vyakula kadhaa ambavyo mama mjamzito anapaswa kuepuka au kula kwa tahadhari kwa sababu vinaweza kuwa na madhara kwa afya yake na mtoto aliye tumboni.
mama mjamzito
Vifuatavyo ni vyakula hatarishi kwa afya ya mama mjamzito ambavyo ni pamoja na:
1) Matunda Na Mboga Zisizooshwa Vizuri.
Matunda na mboga zisizooshwa vizuri zinaweza kubeba mabaki ya dawa za kuulia wadudu na vimelea kama toxoplasma. Safisha vizuri matunda na mboga kabla ya kula.
Matunda Na Mboga Zisizooshwa
kuosha mboga za majani na matunda kabla ya kula
2) Chakula Kibichi Au Kisichoiva Vizuri.
Nyama mbichi au iliyopikwa lakini haikuiva vizuri, samaki mbichi, na mayai mabichi au vyakula vilivyochanganywa na mayai mabichi vinaweza kubeba bakteria na vimelea kama vile salmonella, listeria, na E. coli ambayo ni hatari kwa mama na mtoto.
Mfano: Kuna baadhi ya ‘Ice cream’ na ‘mayonaizi’ hutengenezwa kwa kuchanganywa na mayai mabichi. Mjamzito amekatazwa kuvila vyakula hivyo. Mama mjamzito, Kabla ya kula hakikisha nyama, samaki, na mayai vinaiva vizuri.
3) Pombe.
Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa unywaji wa pombe kiasi kidogo wakati wa ujauzito hauna madhara, kwa maana hiyo matumizi ya pombe hayaruhusiwi kabisa wakati wa ujauzito, hata kama ni kiasi kidogo.
Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito huweza kuathiri ukuaji mzuri wa mtoto. Kutegemeana na kiasi atakachokunywa mjamzito, pombe inaweza kumsababishia mtoto ugonjwa hatari utokanao na pombe maarufu kama Fetal Alcohol Syndrome.
pombe
4) Vinywaji Vyenye Kafeini Nyingi.
Kunywa kafeini kwa kiasi kikubwa kunaweza kuongeza hatari ya kuharibika kwa mimba na matatizo ya ukuaji wa mtoto aliye tumboni. Ingawa kafeini kidogo inaweza kuwa salama ambapo inashauriwa kupunguza ulaji wa kafeini hadi 200 mg kwa siku (karibu kikombe kimoja cha kahawa).
kahawa
5) Samaki Wenye Zebaki Nyingi.
Samaki kama vile papa, chuchunge, swordfish, king mackerel, na tilefish wana kiwango kikubwa cha zebaki ambayo inaweza kuathiri mfumo wa neva wa mtoto. Ulaji wa zebaki kwa wajawazito umehusishwa na uzaaji wa watoto taahira.
Badala yake, chagua samaki wenye kiwango kidogo cha zebaki kama vile salmon, trout, na sardines.
6) Vyakula Vyenye Sukari Na Mafuta Mengi.
Vyakula hivi vinaweza kuchangia kuongeza uzito kupita kiasi na magonjwa kama vile kisukari cha ujauzito, ambayo ni hatari kwa mama na mtoto aliye tumboni.
7) Maziwa Mabichi.
Maziwa mabichi huweza kuwa na bakteria ajulikanae kama ‘Listeria’, ambaye huweza kusababisha kuharibika kwa mimba. Unapokunywa maziwa, hakikisha yamechemshwa au kama ni ya paketi hakikisha ni yale yaliyoandikwa ‘Pasteurized’ na siyo ‘Unpasteurized’.
maziwa mabichi
maziwa yanayochemshwa
HITIMISHO:
Kwa hivyo, ni muhimu kwa mama mjamzito kufuata miongozo ya lishe bora na kushauriana na daktari au mtaalamu wa lishe kuhusu vyakula vinavyofaa kula na vile vya kuepuka.
Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.