Ujue Utando Mweupe Anaozaliwa Nao Mtoto Kwenye Ngozi Na Kazi zake.

Je umewahi kuona mtoto aliyetoka kuzaliwa ana kama vitu vyeupe juu ya ngozi?

Halafu watu wanaanza kusema “labda mama wakati wa ujazito alikula chakula fulani…” au labda mama aliendelea kufanya mapenzi kipindi chote cha ujauzito mpaka anajifungua…”

Kama jibu ni NDIYO, ukweli ni kwamba, hayo maneno hapo juu na mengine mengi yanayosemwa na watu huko mtaani baada ya mtoto kuzaliwa na vitu vyeupe juu ya ngozi yake, hayana uhalisia wowote kwani ni IMANI POTOFU tu.

Hivyo vitu vyeupe unavyoviona juu ya ngozi ya mtoto aliyetoka kuzaliwa sio uchafu, bali kitaalam tunaita vernix caseosa.

Neno hili vernix caseosa linatokana na Kilatini: vernix = “mafuta/varnish” na caseosa = “kama jibini”. Hivyo, vernix caseosa ni kitu cheupe, laini kama krimu au jibini au unaweza ita lotion ya asili kwa mtoto ambayo inafunika ngozi yake akiwa tumboni na hata wakati wa kuzaliwa.

Vernix Caseosa Imetengenezwa Na Nini?

Vernix caseosa ni mchanganyiko wa vitu vitatu vikuu:

1) Mafuta (lipids).

Hutoka kwenye tezi za mafuta za mtoto (sebaceous glands). Mafuta haya hufanya vernix caseosa iwe laini na isiruhusu maji kupenya.

2) Seli Za Ngozi Zilizokufa (Corneocytes).

Hizi ni seli kutoka tabaka la juu la ngozi ambazo husaidia kuunda ule muundo mzito wa vernix caseosa.

3) Maji.

Vernix caseosa ina kiasi kikubwa cha maji (zaidi ya nusu). Hii husaidia kulainisha ngozi ya mtoto.

Pia ina vitu vingine vidogo kama vile:

  • Protini za kinga (antimicrobial proteins)

  • Enzymes zinazosaidia kulinda ngozi

Vernix Caseosa Huzalishwa Kipindi Gani?

Vernix caseosa huanza kutengenezwa wakati wa ujauzito:

  • Huanzia takriban wiki ya 20–24 ya ujauzito

  • Huongezeka zaidi kadri mimba inavyoendelea

  • Hufikia kiwango kikubwa karibu wiki ya 34–38 (karibu na kujifungua)

Kwa watoto:

  • Waliotangulia kuzaliwa (preterm): huwa na vernix caseosa nyingi zaidi

  • Waliochelewa (post-term): huwa na vernix caseosa kidogo au imepungua

Kazi Za Vernix Caseosa:

Vernix caseosa kwa mtoto hufanya kazi zifuatazo;

1) Kinga Ya Ngozi Dhidi Ya Maji Ya Uzazi.

Mtoto hukaa ndani ya maji ya uzazi kwa muda mrefu. Bila vernix caseosa, ngozi ya mtoto ingeweza kulainika kupita kiasi (maceration) lakini pia vernix caseosa hufanya kama kinga ya asili (barrier) kulinda ngozi ya mtoto.

2) Kinga Dhidi Ya Maambukizi.

Vernix caseosa ina kemikali za asili zinazopambana na bakteria na fangasi hivyo husaidia kupunguza hatari ya mtoto kupata maambukizi kabla na baada ya kuzaliwa.

3) Husaidia Wakati Wa Kujifungua.

Vernix caseosa hufanya ngozi ya mtoto kuwa laini na yenye utelezi, hii hupunguza msuguano wakati wa kupita kwenye njia ya uzazi. Hivyo kumrahishishia mama mjamzito wakati kujifungua.

4) Kudhibiti Joto La Mwili.

Baada ya mtoto kuzaliwa, vernix caseosa husaidia mtoto kudumisha joto la mwili (temperature regulation). Lakini pia inasaidia sana kwa watoto wachanga ambao bado hawajakomaa kikamilifu (wamezaliwa kabla ya week 37, yaani preterm babies) kwa kupunguza upotevu wa joto haraka.

5) Kuimarisha Ukuaji Wa Ngozi Ya Mtoto.

Vernix caseosa husaidia kuimarisha ngozi ya mtoto kwa kuifanya iwe na afya na imara baada ya kuzaliwa.

6) Kutoa Unyevu (Moisturizing Effect).

Vernix caseosa ni kama “lotion ya asili” kwa mtoto ambayo hulainisha ngozi ya mtoto na huzuia kukauka.

7) Ina Mchango Katika Mfumo Wa Kinga Wa Mtoto.

Vernix caseosa Ina protini na vitu vinavyosaidia kuandaa mfumo wa kinga wa mtoto.

HITIMISHO:

Vernix caseosa haina uhusiano na chakula alichokula mama wakati wa ujazito, haina uhusiano na tendo la ndoa wakati wa ujauzito, hivyo ukiona mtoto amezaliwa nayo USIHOFU kwani inaweza kuondoka kirahisi baada ya mtoto kuogeshwa au hata ikaisha yenyewe bila shida.

Kwa ushauri na tiba ya magonjwa ya afya ya uzazi wasiliana nasi kwa simu namba 0625 305 487. Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr, Isaya Febu.