- Dr. ISAYA FEBU Newsletter
- Posts
- Soma Hii Kama Unataka Kutibu Ugonjwa Wa Kaswende.
Soma Hii Kama Unataka Kutibu Ugonjwa Wa Kaswende.
Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.
Leo tujifunze kuhusu ugonjwa wa kaswende na jinsi ya kutibu. Ungana nami katika somo hili.
Ugonjwa wa kaswende ni miongoni mwa magonjwa ya zinaa unaosababishwa na maambukizi ya bakteria ambao hujulikana kwa kitaalamu kama Treponema pallidum.
Ugonjwa wa kaswende ambao hujulikana kwa kitaalamu kama syphilis ni ugonjwa hatari sana endapo usipo patiwa matibabu mapema.
kaswende
Mambo Yanayoongeza Hatari Ya Kupata Kaswende:
Unaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa njia zifuatazo;
1) Kufanya ngono isiyo salama na mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huu hasa kupitia mdomo (oral Sex) na mkundu (anal sex).
2) Kuzaliwa na mama ambaye alikuwa na kaswende ya kuambukizwa wakati wa ujauzito.
3) Kupewa damu isiyo salama yenye maambukizi ya bakteria wanaosababisha ugonjwa huu.
Kumbuka: Kushiriki chakula, kukumbatiana, au kutumia bafu moja na mtu aliye na kaswende hakuenezi ugonjwa huo.
Dalili Za Kaswende:
Zifuatazo ni baadhi ya dalili za ugonjwa wa kaswende ambazo ni pamoja na;
1) Vidonda kwenye sehemu za siri hasa kwenye uume, uke au mkundu, mdomoni. Vidonda hivyo hujulikana kama chancre kwa kawaida huwa havina maumivu makali. Unaweza kuvipuuza kwani haviumi na kufikiri vitapona vyenyewe.
2) Vipele kwenye viganja vya mikono na nyayo za miguu ambavyo ni vyekundu au vyekundu-kahawia.
3) Maumivu ya kichwa, mwili na homa.
vipele vya kaswende
Matibabu Ya Kaswende:
Tiba ya kaswende hutegemeana na muda ambao tatizo limedumu.
Zipo dawa aina za vidonge au sindano kulingana na historia na stage (hatua) ya ugonjwa wenyewe. Mfano Penisilini ya Benzathine (Benzathine penicillin) ndiyo chaguo la kwanza la tiba kwa hatua zote za kaswende.
benzathine penicillin
Machaguo mengine, haswa ikiwa mtu aliyeathirika ana mzio (Allergy) wa penisilini, ni doxycycline na ceftriaxone.
Penisilini ya Benzathine kwa kawaida ni sindano inayochomwa kwenye misuli (Intramuscularly), wakati doxycycline na ceftriaxone kwa kawaida huchomwa kwenye mishipa ya damu (Intravenously) au misuli (Intramuscularly).
Dawa zote tatu hutolewa kwa dozi kubwa, kwa siku moja au siku kadhaa mfululizo. Penisilini ya Benzathine inaweza kutolewa katika dozi tofauti, kulingana na hatua iliyofikia kaswende inayotibiwa.
Kumbuka:
Hatua za baadaye za ugonjwa wa kaswende huendelea polepole ndani ya miaka kadhaa na huathiri moyo, ubongo na sehemu nyingine za mwili.
Hii huweza kuonyesha dalili zingine tofauti kama kuishiwa pumzi, kuchanganyikiwa, kusahau, kupoteza uratibu na uharibifu wa neva.
Madhara Ya Kaswende:
Yafuatayo ni madhara yanayoweza kutokea endapo mgonjwa mwenye kaswende hatashindwa kupata matibabu mapema;
1) Matatizo ya kuona hafifu na hata upofu (visual problems, blindness).
2) Kupoteza kusikia (Hearing loss)
3) Uharibifu wa neva (nerves damage)
4) Kupoteza uwezo wa kusimamisha uume (erectile dysfunction)
5) Matatizo ya moyo na mishipa ya damu (heart problems)
6) Kiharusi (stroke)
HITIMISHO:
Tembelea kituo cha afya kilichokaribu nawe pima na upatiwe matibabu wewe pamoja na mwenza wako.
Kujifunza zaidi kuhusu afya tembelea tovuti yangu: HOME | ISAYA FEBU
Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.