Tatizo La Kuota Ndevu Kwa Wanawake Na Jinsi Ya Kutibu.

Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.

Je umeshawahi kukutana na mwanamke mwenye ndevu nyingi? Bila shaka, jibu ni NDIYO.

hirsutism

Hilo ni tatizo la kiafya ambalo hujulikana kwa kitaalamu kama Hirsutism.

Leo tujifunze kuhusu sababu za tatizo hilo na jinsi ya kutibu.

Hirsutism ni hali ambapo wanawake wanakua na ukuaji wa nywele wenye kufanana na wa wanaume katika maeneo ambayo kwa kawaida wanawake hukua na nywele kidogo au hazikui kabisa kama vile usoni, kifuani, tumboni.

Takwimu zinaonesha 5%-10% ya wanawake duniani wanatatizo ili hasa maeneo ya Ulaya, Africa na Asia.

Sababu Za Hirsutism:

Tatizo ili husababishwa na vyanzo mbalimbali huku chanzo mama kikiwa ni mvurugiko wa homoni ndani ya mwili ambapo hupelekea homoni za kiume (androgens) kuongezeka ikiwemo testosteroni na kupelekea nywele kuongezeka. Sababu zingine zinazopelekalea tatizo hili ni pamoja na:

1) Magonjwa Ya Ovari.

Magonjwa ya ovari kama vile Polycystic Ovarian Syndrome (PCOS) yanaweza kusababisha hirsutism kwa sababu ya mabadiliko ya homoni yanayotokea. Katika PCOS, ovari zinaweza kuzalisha kiwango kikubwa cha homoni za kiume (androgens).

2) Matumizi Ya Baadhi Ya Dawa.

Baadhi ya dawa, kama vile dawa za homoni au dawa zingine kama vile minoxidil, steroids zinaweza kusababisha hirsutism kama athari tarajiwa (side effect).

3) Urithi.

Hirsutism inaweza kuwa ya kurithi katika familia fulani. Kama wanafamilia wengine wana historia ya hirsutism (uwepo wa wanawake wenye shida hii katika familia ya mwanamke), kuna uwezekano mkubwa wa mwanamke kupata hali hiyo.

4) Unene Kupita Kiasi.

Unene kupita kiasi unaweza kusababisha ongezeko la homoni za kiume mwilini, hali ambayo inaweza kusababisha hirsutism.

5) Matatizo Ya Tezi.

Matatizo ya tezi, kama vile matatizo katika tezi ya adrenali au tezi ya pituitari, yanaweza kusababisha mabadiliko katika viwango vya homoni mwilini na kusababisha hirsutism. Tezi ya adrenali na tezi ya pituitari zinahusika katika kudhibiti uzalishaji wa homoni mbalimbali mwilini, ikiwa ni pamoja na homoni za kiume (androgens) kama vile testosterone.

Tiba Ya Hirsutism:

Ukiachana na kunyoa nywele hizo, tatizo hili linaweza kutibika kama ifuatavyo:

1) Mabadiliko Ya Mtindo Wa Maisha.

Kwa baadhi ya wanawake hasa wenye unene kupita kiasi, mabadiliko katika mtindo wa maisha kama vile lishe bora na mazoezi ya mara kwa mara yanaweza kusaidia kupunguza dalili za hirsutism. Kwa mfano, lishe yenye afya inaweza kusaidia kudhibiti uzito wa mwili na kupunguza viwango vya homoni zinazohusika katika hirsutism.

2) Dawa Za Kupunguza Homoni Za Kiume.

Daktari anaweza kuagiza dawa za kupunguza homoni za kiume (androgen blockers) au dawa za kudhibiti uzalishaji wa homoni za kiume katika mwili ili kupunguza ukuaji wa nywele wa kiume. Dawa hizi zinaweza kusaidia kudhibiti hirsutism kwa kuzuia athari za homoni za kiume kwenye follicles za nywele.

3) Matibabu Ya Kuondoa Nywele.

Matibabu kama vile laser hair removal au electrolysis hair removal yanaweza kutumika kwa mafanikio katika kuondoa nywele zilizoathiriwa na hirsutism. Matibabu haya yanaweza kusaidia kupunguza ukuaji wa nywele na kuboresha muonekano wa ngozi.

Lakini pia matibabu yanaweza kuhusisha matumizi ya creams zitakazo sababisha nywele zisiote kama eflornithine cream.

4) Matibabu Ya Homoni.

Kwa wanawake wenye hirsutism kutokana na matatizo ya homoni kama vile PCOS, matibabu ya homoni yanaweza kusaidia kudhibiti mzunguko wa hedhi na viwango vya homoni mwilini, hivyo kupunguza dalili za hirsutism.

5) Upasuaji.

Katika kesi nadra sana ambapo hirsutism inasababishwa na matatizo ya tezi kama vile pituitary adenoma, upasuaji wa tezi unaweza kuhitajika kurekebisha tatizo hilo.

HITIMISHO:

Kujifunza zaidi kuhusu afya tembelea tovuti yangu: HOME | ISAYA FEBU

Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.