Hizi Ndio Sababu 9 Zinazochangia Matiti Ya Akina Mama Kulala.

Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.

Leo tujifunze kuhusu sababu zinazochangia matiti ya akina mama kulala. Ungana nami katika somo hili.

Kabla ya kufahamu kwa nini matiti ya akina mama hulala, ni vyema kufahamu muudo wa titi la mwanamke.

Matiti yameundwa na tezi za kuzalisha maziwa ambazo zipo kama mafuta, zimeunganishwa na mirija ya kusafirisha maziwa, kuna tishu za mafuta yanayoongezea ujazo, kuna ligaments zinazoshikiria maziwa, chuchu na ngozi ya juu. 

Ukubwa na umbo la matiti hutegemea na chembechembe za urithi ulizopata toka Kwa wazazi, uzito wako wa mwili, kiwango chako cha homoni, lishe yako, umri wako na idadi za mimba ulizowahi kubeba.

Mwanamke Anapopata Ujauzito Umbo La Matiti Hubadilika.

Mwanamke anapobeba ujauzito mwili wake hufanya mabadiliko makubwa ili kuweza kuhudumia mtoto akiwa tumboni na mara atakapozaliwa. Moja ya viungo ambavyo hupata mabadiliko ni matiti; homoni zinazotolewa na mwili wakati wa ujauzito huchochea mabadiliko wakati wa ujauzito na kujifungua.

Mabadiliko yanayojitokeza kwenye maziwa wakati wa ujauzito ni pamoja na: Maziwa kujaa, kujitokeza kwa mishipa ya damu kwenye ngozi ya titi, chuchu kukolea rangi.

Je Unaponyonyesha Mtoto Matiti Uharibika Na Kulala?

Unaweza jiuliza kwa nini kuna kampeni nyingi za kuhamasisha akina mama kunyonyesha watoto wao? Jibu rahisi unalohitaji kufahamu ni kwamba maziwa ya mama ndicho chakula bora zaidi ambacho mtoto mchanga anaweza kupata.

Maziwa mbadala yote kama vile maziwa ya ng’ombe au maziwa ya kopo huwa ni duni ukilinganisha na maziwa ya mama.

Daktari mtaalamu wa upasuaji wa matiti ya wanawake Dr Rinker aliamua kufanyia utafiti malalamiko mengi kutoka kwa wateja wake kuwa matiti yao yamelala kutokana na wao kunyonyesha watoto wao. Malalamiko kama hayo pia yapo katika mazingira yetu hasa kwa wanawake ambao bado wana umri mdogo hivyo huogopa kunyonyesha wakihofia matiti yao kulala.

Kutokana na utafiti wa Dr Rinker na watafiti wengine imeonekana kuwa unyonyeshaji hausababishi matiti ya akina mama kulala; matiti hulala kutokana na sababu mbalimbali.

Sababu Zinazochangia Matiti Ya Akina mama Kulala:

Kuna sababu mbalimbali zinazochangia matiti ya akina mama kulala, baadhi ya sababu hizo ni pamoja na:

1) Urithi.

Matiti huweza kulala sio kwa sababu unamnyonyesha mwanao bali kwa sababu ya chembe zako za urithi (genes). Chembe za urithi huwa ndo zinaamua ukubwa wa matiti ya mwanamke, pia ndo huamua uimara wa tishu zinazoshikiria matiti.

Baadhi ya wanawake kiasili huwa na tishu imara ambazo hufanya matiti yasimame, wengine huwa na tishu ambazo ni dhaifu hivyo matiti huwahi kulala. Kuna wanawake wana maradhi ya kurithi ambayo huathiri uimara ya tishu aina ya ligaments ambazo zinashikiria matiti. Mfano ugonjwa uitwao Ehler’s Danlos syndrome.

2) Ukubwa Wa Matiti.

Kutokana na ujazo na uzito, matiti makubwa huwa rahisi kulala. Hali hii sio tatizo la kiafya bali ni hali ya kawaida ya matiti kukaa kulingana na uzito wake (normal variation).

3) Umri.

Matiti yameshikiliwa kwenye kifua na kiwambo kinachoitwa cooper’s ligament. Kadri umri unavyokwenda hiki kiwambo hulegea na kupoteza nguvu ya kushikiria matiti. Sababu nyingine ni kwamba baada ya mwanamke kufikia ukomo wa hedhi (Menopause) tishu ndani ya matiti husinyaa hii hutokana na kushuka kwa homoni kama estrojeni ambayo husaidia kufanya matiti yajae.

4) Uvutaji Wa Sigara.

Sigara hutoa kemikali ambazo huingia kwenye damu na kwenda kuharibu kampaundi inayoitwa elastin ambayo ina kazi ya kufanya ngozi iwe nyororo na inayovutika. Sigara ikiharibu kampaundi hii kwenye ngozi; ngozi ya matiti huwa dhaifu na kuzeeka hivyo hushindwa kushikiria titi vizuri, na titi hulala na kuwa tepetepe.

5) Upungufu Wa Vitamin C.

Vitamin C ni kirutubisho muhimu kwenye mwili ambacho hutumika kutengeneza kitu kinaitwa Collagen. Collagen ni kama malighafi inayotumika kutengeneza ngozi ya mwili, mishipa ya damu , viwambo vinavyoshikiria matiti.

Iwapo mwanamke ana upungufu ya vitamini C ngozi yake itakuwa dhaifu pia na Cooper's ligament (inayoshikiria maziwa) itakuwa dhaifu na matiti yatalala. Machungwa ni moja ya vyakula vyenye vitamin C ya kutosha.

6) Mazoezi Ya Kukimbia Au Kurukaruka Bila Kuvaa Bra Za Michezo.

Akina mama wanapokimbia maziwa huruka juu, chini na pembeni. Iwapo mwanamke anafanya mazoezi au kukimbia bila kuvaa bra ya michezo kuruka ruka kwa matiti husababisha Cooper's ligament ivutike na kuwa dhaifu baada ya muda na kusababisha maziwa kulala.

Bra za michezo hubana maziwa yatulie sehemu moja hivyo huzuia yasiruke wakati unafanya mazoezi.

7) Kuacha Kunyonyesha Ghafla.

Wakati wa ujauzito matiti hujaa, pia mtoto anaponyonya matiti hujaa zaidi ili kutengeneza maziwa zaidi. Inapotokea mama kaacha ghafla kumnyonyesha mtoto; tishu zinazotengeneza maziwa husinyaa lakini ngozi ya nje haitasinyaa na kusababisha matiti kuwa na muonekano tepetepe.

AKina mama wanaonyonyesha inabidi wajifunze namna ya kuachisha mtoto kunyonya anapofikisha miaka 2. Mtoto anatakiwa aachishwe kunyonya taratibu ili kuleta kitu kinaitwa “Breast Involution” Yaani titi kunywea taratibu na kuwa dogo kama lilivyokuwa kabla ya ujauzito.

8) Idadi Ya Mimba Ulizowahi Kubeba.

Wakati wa ujauzito mwili huandaa matiti kuwa tayari kunyonyesha; Tishu zinazohusika na uzalishaji maziwa hukua na kuwa kubwa.

Baada ya kujifungua na kumaliza kunyonyesha matiti hupungua ukubwa ili kurudi kwenye umbo lake lilivyokuwa kabla ya ujauzito. Matiti yanaporudi kwenye umbo la zamani hulala kwa kiasi tofauti na ulivyokuwa kabla ya kubeba ujauzito bila kujali umebeba ujauzito bado Binti mdogo au mtu mzima.
Kila mara unapobeba ujauzito hali hujirudia na matiti huzidi kulala.

9) Mabadiriko Ya Uzito.

Matiti yametengenezwa na tishu nyingi za mafuta, unapo nenepa na tishu hizo hunenepa, ambapo husababisha maziwa kukua na kuongezeka ukubwa hivyo huweza kulala kwa kiasi.

Pia matiti hulala kwa akina mama waliopungua (kukonda) ghafla hupata shida ya matiti kuonekana yamelala, unapopungua ghafla tishu za ndani za maziwa hupungua pia lakini ngozi ya nje hubaki na ukubwa uleule hivyo kusababisha kupwaya na titi kuonekana limelala.

HITIMISHO:

Kujifunza zaidi kuhusu afya tembelea tovuti yangu: HOME | ISAYA FEBU

Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.