- Dr. ISAYA FEBU Newsletter
- Posts
- Sababu Za Kifafa Cha Mimba.
Sababu Za Kifafa Cha Mimba.
Kifafa Cha Mimba Ni Nini?
Kifafa cha mimba ambacho kinajulikana kwa kitaalamu kama pre-eclampsia ni hali ya dharura (medical emergency condition) inayojitokeza baada ya wiki ya 20 ya ujauzito, ambapo mama mjamzito hupata shinikizo la juu la damu (hypertension) pamoja na dalili kama vile protini kwenye mkojo (proteinuria), kuvimba kwa mwili (edema) hasa uso na mikono, maumivu ya kichwa (headache), na matatizo ya kuona (blurred vision).
Kifafa cha mimba pia kinaweza kutokea baada ya kujifungua (mara nyingi ndani ya masaa 48 ya kujifungua mpaka wiki 6 baada ya kujifungua) ambacho hujulikana kwa kitaalamu kama postpartum pre-eclampsia.
Kifafa cha mimba au wengine wanakiita kifafa cha uzazi ni miongoni mwa matatizo yanayosababisha vifo vya wajawazito nchini.

Sababu halisi ya kifafa cha mimba haijulikani wazi, lakini kuna mambo kadhaa yanayoweza kuongeza hatari ya kupata hali hii ambayo ni pamoja na:
1) Shinikizo La Juu La Damu (Hypertension).
Wanawake wenye shinikizo la juu la damu kabla au wakati wa ujauzito wako kwenye hatari kubwa ya kupata kifafa cha mimba.

2) Ujauzito Wa Mapacha Au Zaidi.
Kuwa na mimba ya watoto wawili (twins) au zaidi huongeza mzigo kwa mwili wa mama (increase placental mass) na kuongeza hatari ya kupata kifafa cha mimba.

3) Umri Wa Mama Mjamzito.
Wanawake walio chini ya miaka 20 au zaidi ya miaka 40 wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kifafa cha mimba.
4) Historia Ya Kifafa Cha Mimba.
Ikiwa mama aliwahi kupata kifafa cha mimba katika ujauzito wa awali, ana uwezekano mkubwa wa kupata kifafa hicho tena katika mimba zinazofuata.
5) Kuwa Na Ujauzito Wa Kwanza (Primigravidity).
Wanawake wanaopata mimba kwa mara ya kwanza (primigravida) wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kifafa cha mimba.
6) Historia Ya Kifafa Cha Mimba Kwenye Familia.
Kama mama au dada yako aliwahi kupata kifafa cha mimba, unakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata kifafa hicho.
7) Unene Kupita Kiasi (Obesity).
Unene kupita kiasi huongeza hatari ya kupata shinikizo la juu la damu, ambalo ni sababu kuu ya kifafa cha mimba.

8) Magonjwa Mengine Sugu Kwa Mama Mjamzito.
Magonjwa mengine sugu kwa mama mjamzito kama vile kisukari, magonjwa ya figo, na matatizo ya autoimmune (autoimmune disorders) yanaweza kuongeza hatari ya kupata kifafa cha mimba.

Figo zikishindwa kufanya kazi ipasavyo, zinaweza kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la damu na protini kwenye mkojo.
HITIMISHO:
Matibabu ya kifafa cha mimba yanahitaji uangalizi wa haraka na mara nyingi inahusisha kujifungua mapema ili kuzuia madhara zaidi kwa mama na mtoto.