Lijue Tatizo La Kujihisi Mnene Na Kukosa Hamu Ya Kula (Anorexia nervosa).

Anorexia Nervosa Ni Nini?

Anorexia Nervosa ni tatizo la akili na lishe (eating disorder) ambapo mtu hujizuia kula chakula au kula kidogo sana kwa hofu kubwa ya kunenepa, hata kama tayari ni mwembamba kupita kiasi. 

Mtu mwenye anorexia huwa na mtazamo usio sahihi juu ya mwili wake na huamini kuwa bado ni mnene hata anapokonda kupita kiasi.

Dalili Za Anorexia Nervosa:

Dalili za anorexia nervosa ni pamoja na:

1) Kukonda kupita kiasi (BMI chini ya kiwango cha kawaida)

2) Uso na mwili kuwa wa kuchoka au kuzeeka mapema

3) Ngozi kuwa kavu, nywele kukatika au kudondoka

4) Baridi kupita kiasi hata kama hali ya hewa ni ya kawaida

5) Kula chakula kidogo sana au kuepuka kabisa baadhi ya vyakula

6) Kupima uzito mara kwa mara

7) Hofu ya kunenepa hata kama mtu ni mwembamba sana

8) Kujificha kula au kusema “nimeshiba” kila wakati

9) Kufanya mazoezi kupita kiasi bila kupumzika

10) Kukataa kula mbele za watu

11) Kukosa hedhi kwa wanawake (amenorrhea)

12) Udhaifu wa misuli

13) Mapigo ya moyo kuwa ya polepole au yasiyo ya kawaida

14) Kukosa usingizi au kupata usingizi hafifu

15) Upungufu wa damu na madini mwilini

Sababu Zinazochangia Anorexia Nervosa:

Sababu zinazochangia kupata anorexia nervosa ni pamoja na:

1) Shinikizo La Kijamii/Kidijitali.

Mitazamo ya urembo wa “mwili mwembamba” inayochochewa na mitandao ya kijamii au mitindo. Kwa mfano jamii inayoamini urembo wa msichana huongezeka anapokuwa mwembamba ina hatari ya kuzalisha wagonjwa wengi wa tatizo hili kuliko ile inayoamini tofauti.

2) Magonjwa Ya Akili.

Wasiwasi (anxiety), huzuni ya muda mrefu (depression), au matatizo ya kujithamini.

3) Mazingira Ya Familia.

Familia zinazosisitiza sana uzito, mafanikio au nidhamu kali.

4) Maisha Ya Ushindani.

Kwa mfano, wanamitindo, wanariadha au wacheza dansi huathirika zaidi.

Matibabu Ya Anorexia Nervosa:

Anorexia ni ugonjwa unaohitaji matibabu ya pamoja kutoka kwa wataalamu wa afya ya akili, lishe, na daktari wa mwili. Matibabu ni pamoja na:

1) Ushauri Wa Kisaikolojia (Psychotherapy).

Hususan CBT (Cognitive Behavioral Therapy).

Cognitive Behavioral Therapy (CBT) ni aina ya tiba ya kisaikolojia (psychotherapy) inayosaidia mtu kubadili namna anavyofikiri (cognitive) na kutenda (behavioral) ili kuondoa matatizo ya kihisia, kisaikolojia au tabia.

Kwa mgonjwa wa anorexia nervosa, CBT husaidia kubadili jinsi mgonjwa anavyofikiri kuhusu:

  • Mwili wake

  • Uzito wake

  • Chakula

  • Thamani yake binafsi

2) Msaada Wa Lishe.

Kurejesha uzito kwa mpangilio na kwa usimamizi wa mtaalamu wa lishe.

3) Dawa.

Kama antidepressants au mood stabilizers ikiwa kuna msongo wa mawazo.

4) Huduma Ya Familia.

Ushirikiano wa familia katika kuunga mkono mgonjwa kwa lengo la kuhakikisha anakuwa sawa kiafya.

Madhara Ya Anorexia Nervosa:

Madhara yatokanayo na anorexia nervosa ni pamoja na:

1) Kudhoofika kwa moyo na ini

2) Kukosa uwezo wa kushika mimba (kwa wanawake)

3) Kupoteza nguvu za mwili na akili

4) Uwezekano mkubwa wa kufa kutokana na njaa au matatizo ya moyo (Anorexia ina kiwango cha vifo cha juu zaidi kati ya magonjwa ya akili)

HITIMISHO:

Anorexia Nervosa ni tatizo la kiafya linaloweza kuwa hatari sana ikiwa halitashughulikiwa mapema. Ni muhimu kutambua dalili zake mapema na kumsaidia mtu anayeshiriki tabia za kujinyima chakula, kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Jambo La Kuzingatia:

Zungumza na daktari iwapo una ndugu au mtu wa karibu ambaye:

1) Ana hisia zisizo za kawaida kuhusu uzito wake

2) Anafanya mazoezi kupita kiasi

3) Anajiwekea kikomo kisicho cha kawaida katika kiwango cha ulaji wake

4) Ana uzito wa chini kuliko kawaida