Kijue Kifafa Cha Mimba, Dalili, Tiba Na Madhara Yake.

Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.

Leo tujifunze kuhusu kifafa cha mimba na madhara yake kwa mwanamke mjamzito. Ungana nami katika somo hili.

Kifafa cha mimba, ambacho pia hujulikana kwa kitaalamu kama pre-eclampsia, ni hali inayotokea wakati wa ujauzito na inaathiri asilimia ndogo ya wanawake wajawazito. Kifafa cha mimba kinaweza kuwa na athari mbaya kwa mama na mtoto ikiwa hakitatibiwa.

Sababu Za Kifafa Cha Mimba:

Sababu kamili za kifafa cha mimba hazijulikani, lakini kuna mambo kadhaa yanayohusishwa na hatari kubwa ya kupata hali hii ikiwemo:

1) Historia Ya Kuugua Kifafa Cha Mimba.

Wanawake ambao wamewahi kuwa na kifafa cha mimba katika ujauzito wa awali wako kwenye hatari kubwa ya kupata tena hali hii.

2) Mimba Ya Kwanza.

Wanawake ambao ni wajawazito kwa mara ya kwanza (primigravida) wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kifafa cha mimba.

3) Historia Ya Kifafa Cha Mimba Katika Familia.

Ikiwa mama au dada yako alipata kifafa cha mimba, una uwezekano mkubwa wa kupata hali hii.

4) Umri.

Wanawake walio na umri wa chini ya miaka 20 au zaidi ya miaka 40 wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kifafa cha mimba.

5) Uzito Kupita Kiasi.

Uzito mkubwa (obesity) huongeza hatari ya kifafa cha mimba. BMI (Body Mass Index) ya juu inahusishwa na ongezeko la hatari ya kupata kifafa cha mimba.

6) Mimba Za Mapacha Au Zaidi.

Wanawake wanaobeba watoto mapacha au zaidi (multiple gestation) wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kifafa cha mimba.

7) Magonjwa Mengine.

Wanawake wenye magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu (hypertension), magonjwa ya figo, na baadhi ya magonjwa ya kinga mwilini wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata kifafa cha mimba.

Dalili Za Kifafa Cha Mimba:

Dalili za kifafa cha mimba ni pamoja na:

1) Shinikizo la damu kupanda (hypertension)

2) Kuvimba kwa mikono na uso (edema)

3) Protini kwenye mkojo (proteinuria)

4) Kuona giza au kutoona vizuri (blurred vision).

5) Maumivu makali ya kichwa (severe headache)

6) Kichefuchefu na kutapika

Kumbuka: Mara nyingi kifafa cha mimba hutokea kwa mimba yenye umri wa wiki 20 na zaidi, na inaweza itokee wakati wa ujauzito au mara tu baada ya kujifungua.

Matibabu Na Jinsi Ya Kujikinga Na Kifafa Cha Mimba:

Matibabu na jinsi ya kujikinga na kifafa cha mimba yanahusisha mambo yafuatayo:

1) Kudhibiti Shinikizo La Damu.

Dawa za kushusha shinikizo la juu la damu mfano methyldopa zinaweza kutumika kusaidia kudhibiti kiwango cha shinikizo la damu kwa wanawake walio katika hatari kubwa.

2) Ufuatiliaji Wa Mara Kwa Mara Wa Afya.

Wanawake wajawazito wanapaswa kwenda kwa daktari wao kwa ajili ya uchunguzi wa mara kwa mara kwa ili kufuatilia shinikizo la damu na dalili zingine za kifafa cha mimba.

3) Lishe Bora Na Mazoezi.

Kula chakula bora na kufanya mazoezi kwa kawaida inaweza kusaidia kudhibiti uzito na shinikizo la damu.

4) Kujifungua Mapema.

Katika visa vya kifafa cha mimba kilicho katika hali mbaya zaidi (severe pre eclampsia), kujifungua mapema (kwa njia ya upasuaji au kawaida) inaweza kupendekezwa ili kuzuia matatizo zaidi kwa mama na mtoto.

Madhara Ya Kifafa Cha Mimba:

Yafuatayo ni madhara yanayoweza kutokea endapo mama mjamzito mwenye kifafa cha mimba atashindwa kupata matibabu haraka ambayo ni pamoja na:

1) Wakati wa kifafa cha mimba kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kondo la nyuma (placenta) kubanduka na kutoka kwenye mfuko wa uzazi, hali hii kwa kitalaamu hujulikana kama placental abruption ambapo mwanamke mwenye tatizo hili hutokwa damu nyingi zaidi na hata kupelekea kifo.

2) Uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa njiti na matatizo yanayoambatana na hali hiyo huongezeka.

3) Mgonjwa anaweza kupata tatizo la damu kushindwa kuganda linaloitwa disseminated intravascular coagulation (DIC). Tatizo hili linaweza kusababisha mama kuvuja damu nyingi na hata kufa.

HITIMISHO:

Kama ilivyoandikwa hapo juu, kifafa cha mimba ni ugonjwa wa dharura (medical emergency condition), hivyo basi mama mjamzito mwenye tatizo hili analazimika kuwaishwa haraka hospitali ili kunusuru afya yake na mtoto aliye tumboni.

Kujifunza zaidi kuhusu afya tembelea tovuti yangu: HOME | ISAYA FEBU

Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.