Ijue Njia Ya Uzazi Wa Mpango Ya Kumwaga Nje Shahawa.

Njia ya uzazi wa mpango ya kumwaga nje shahawa inayojuliakana pia kwa kitaalamu kama withdrawal method/pulling out method ni ni mbinu ya uzazi wa mpango inayotegemea mwanaume kutoa uume wake kutoka kwenye uke wa mwenza wake kabla ya kufikia kileleni (kumwaga shahawa) wakati wa tendo la ndoa  ili kuhakikisha kwamba shahawa haziingii ndani ya uke.

Lengo la njia hii ni kuzuia mbegu za kiume kufika kwenye yai la mwanamke (ovum), hivyo kuzuia mimba kutungwa hasa pale mwanamke anaposhiriki tendo la ndoa siku za hatari.

Jinsi Njia Hii Ya Uzazi Wa Mpango Inavyofanya Kazi:

Mwanaume anatakiwa kuwa na udhibiti wa hali ya juu wa mwili wake na kutoa uume kutoka kwenye uke mara tu anapohisi anakaribia kufika kileleni (perfect timing).

Ni muhimu shahawa zote zimwagwe nje ya uke kwani shahawa zinapomwagwa nje ya uke uwezekano wa mbegu za kiume kufika kwenye mfuko wa uzazi unapungua.

Ufanisi Wa Njia Ya Kumwaga Nje Shahawa:

Ufanisi wa njia hii ya uzazi wa mpango hujumuisha mambo yafuatayo:

1) Ufanisi Wa Kawaida.

Takriban 78%, ikimaanisha kwamba kati ya wanawake 100 wanaotumia njia hii kwa mwaka mmoja, takriban 22 wanaweza kushika mimba.

2) Ufanisi Wa Hali Ya Juu.

Ikiwa inatumiwa kikamilifu (bila makosa), inaweza kufikia ufanisi wa hadi 96%, lakini ni nadra kufanikisha kiwango hiki kwa sababu ya makosa ya binadamu.

Changamoto Zinazoweza Kuathiri Ufanisi Wa Njia Hii Ya Uzazi Wa Mpango:

Njia ya hii ya uzazi wa mpango inaweza kuathiriwa na changamoto zifuatazo:

1) Majimaji Ya Awali Ya Shahawa (Pre-Ejaculate).

Majimaji yanayotoka kabla ya mshindo (pre-ejculate) yanaweza kuwa na mbegu za kiume (ingawa kiwango chake ni kidogo) zinazoweza kusababisha mimba.

2) Kuchelewa Kutoa Uume Kutoka Kwenye Uke.

Ikiwa mwanaume hatatoa uume kutoka kwenye uke kwa wakati (perfect timing), hata tone dogo la shahawa linaweza kusababisha mimba.

3) Kuwepo Kwa Mbegu Za Kiume Kwenye Uume.

Ikiwa mwanaume alishamwaga shahawa awali na hajakojoa kabla ya tendo lingine, mbegu za kiume zinazobaki kwenye mrija wa mkojo (urethra) zinaweza kusababisha mimba.

Faida za Njia ya Kumwaga Nje Shahawa:

Njia hii ya uzazi wa mpango hujumuisha faida zifuatazo:

1) Hakuna Gharama.

Hii ni njia ya bure, haina hitaji la vifaa maalum.

2) Haina Athari Za Kiafya.

Haijumuishi kemikali au homoni zinazoweza kusababisha madhara ya kiafya.

3) Inapatikana Wakati Wowote.

Unaweza kuitumia bila maandalizi ya awali.

Hasara Za Njia Ya Kumwaga Nje Shahawa:

Zifuatazo ni hasara za njia hii ya uzazi wa mpango ambazo ni pamoja na:

1) Ufanisi Mdogo.

Ufanisi wake si wa uhakika, hasa ikiwa itatumika vibaya na uwezekano wa kushindwa ni mkubwa.

 2) Inahitaji Udhibiti Mkubwa.

Mwanaume anatakiwa kuwa na uwezo mzuri wa kudhibiti (control) wakati wa kutoa uume ukeni, jambo ambalo si rahisi kwa kila mtu.

3) Hatari Ya Magonjwa Ya Zinaa (STIs).

Njia hii haizuii maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile VVU, kisonono, au kaswende.

HITIMISHO:

Njia ya kumwaga nje inaweza kuwa na ufanisi wa wastani, lakini kwa ulinzi bora zaidi dhidi ya mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa, unashauriwa kutumia njia salama zaidi kama kondomu, vidonge vya uzazi wa mpango, au sindano.