- Dr. ISAYA FEBU Newsletter
- Posts
- Faida Ya Tendo La Ndoa Kwa Mjamzito.
Faida Ya Tendo La Ndoa Kwa Mjamzito.
Tendo La Ndoa:
Kwa kawaida, tendo la ndoa wakati wa ujauzito ni salama kwa wanawake wengi ikiwa ujauzito wao hauna matatizo. Wanandoa wengi wanaendelea kufurahia uhusiano wa kimapenzi wakati huu, ingawa mabadiliko ya kimwili na kihisia yanaweza kuathiri tamaa na faraja wakati wa tendo hilo.
Tendo la ndoa wakati wa ujauzito linaweza kuwa na faida kadhaa, si tu kwa afya ya mama, bali pia kwa uhusiano kati ya wenzi.
Leo katika mada yetu tutazungumzia baadhi ya faida za kushiriki tendo la ndoa kwa mama mjamzito. Ungana nami katika kuchambua faida hizi.
1) Kupunguza Msongo Wa Mawazo.
Tendo la ndoa huchochea utolewaji wa homoni za furaha kama vile endorphins na oxytocin, ambazo hupunguza msongo wa mawazo (stress) na kuleta hisia za furaha. Hii humsaidia mjamzito kujisikia vizuri hali ambayo huboresha uhusiano na mwenza wake.
2) Kuboresha Mzunguko Wa Damu.
Tendo la ndoa linaweza kusaidia kuboresha mzunguko wa damu, jambo ambalo ni muhimu wakati wa ujauzito. Mzunguko mzuri wa damu husaidia kusafirisha virutubisho kwa mtoto aliye tumboni na kuboresha afya ya mama.
3) Kuimarisha Mfumo Wa Kinga Ya Mwili.
Kufanya mapenzi mara kwa mara kunaweza kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili kwa kuongeza uzalishaji wa antibodies kama vile immunoglobulin A (IgA), ambayo husaidia mwili kupambana na maambukizi. Hii ni muhimu hasa kwa mjamzito ili kumlinda yeye na mtoto aliyetumboni.
4) Kuboresha Usingizi.
Wanawake wajawazito mara nyingi hukumbwa na matatizo ya usingizi kutokana na mabadiliko ya homoni na mwili. Baada ya kufika kileleni (orgasm), baadhi ya wanawake hupata usingizi mzuri kutokana na homoni kama vile oxytocin na prolactin zinazozalishwa.
5) Kuimarisha Misuli Ya Nyonga (Pelvic Floor Muscles).
Kufanya tendo la ndoa husaidia kuimarisha misuli ya nyonga, ambayo ni muhimu kwa ajili ya kumsaidia mwanamke mjamzito wakati wa kujifungua.
6) Kuboresha Uhusiano Wa Kimapenzi.
Wakati wa ujauzito, tendo la ndoa linaweza kusaidia kudumisha ukaribu wa kihisia kati ya wenza. Mabadiliko ya mwili na homoni yanaweza kuathiri hisia za mwanamke, lakini tendo la ndoa linalofanywa kwa upendo linaweza kusaidia kuimarisha uhusiano.
7) Kupunguza shinikizo la damu.
Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa tendo la ndoa linaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu kwa muda mfupi, jambo ambalo ni muhimu kwa mjamzito ili kuzuia matatizo kama vile kifafa cha mimba (pre-eclampsia)
8) Kuchochea Maandalizi Ya Mwili Kwa Ajili Ya Kujifungua.
Kusisimka na kufika kileleni wakati wa tendo la ndoa kunaweza kuchochea mikazo midogo ya misuli ya uterasi (braxton hicks contraction). Hii siyo hatari kwa mwanamke mwenye ujauzito wenye afya, bali inasaidia mwili kujiandaa kwa kujifungua kwa namna ya kawaida (spontaneous vaginal delivery). Pia, shahawa za mwanaume zina prostaglandins, ambazo zinaweza kusaidia katika kulainisha (ripening) mlango wa kizazi kwa ajili ya leba wakati unapokaribia kujifungua.
Mikao ya kushiriki tendo la ndoa (sex positions) inayoshauriwa kutumika kwa mjamzito.
HITIMISHO:
Ingawa kuna faida nyingi za kushiriki tendo la ndoa wakati wa ujauzito, ni muhimu kuzingatia usalama wa afya ya mjamzito. Unapopata dalili kama vile kutokwa na damu ukeni (per vaginal bleeding), maumivu makali wakati wa tendo la ndoa (dyspareunia), au matatizo yoyote wakati wa kushiriki tendo la ndoa, ni vyema kumwona daktari. Pia, baadhi ya hali za kiafya, kama vile placenta previa, zinaweza kumfanya mjamzito asishiriki tendo la ndoa kwa usalama wake na wa mtoto aliyetumboni.