- Dr. ISAYA FEBU Newsletter
- Posts
- Hii Ndio Elimu Muhimu Sana Usiyoijua Kuhusu Bidhaa Za Plastiki Na Afya Yako.
Hii Ndio Elimu Muhimu Sana Usiyoijua Kuhusu Bidhaa Za Plastiki Na Afya Yako.
Hello habari yako, natumaini unaendelea vizuri.
Leo tujifunze somo kuhusu matumizi ya bidhaa za plastiki na afya yako . Ungana nami katika somo hili.
Kuna elimu muhimu sana kuhusu bidhaa za plastiki ambayo ni muhimu kujua ili kuendelea kulinda afya yako.
Sio kwamba plastiki zote ni sawa; zinatofautiana kemikali zilizonazo na uwezekano wa kutumika zaidi ya mara moja. Kila plastiki ina alama zinazoitwa "Resin Code"
Unaweza angalia kama plastiki unayotumia ni salama kwa matumizi zaidi ya mara moja, ina aina gani ya plastiki nk, kwa kuangalia resin code kwenye kitako cha plastiki hiyo. Elimu hii wengi wa watumiaji hatuna ndio maana nimeamua kuandika.
Vilevile athari ya hizi plastiki kiafya bado shahidi za kisayansi na tafiti bado hazitoshi. Ni muhimu kwa wanasayansi wetu ndani kuziangalia na kushauri jamii vilevile watengezaji plastiki.
Kuhusu namba hii
Nambari ya Kutambua Resini (RIC) ni namba muhimu ya kutambua na kuelewa aina tofauti za plastiki zinazotumiwa katika bidhaa mbalimbali.
Nambari hizi, zinazowakilishwa na nambari ndani ya pembetatu kutoka 1 hadi 7, zinaashiria muundo wa resin wa nyenzo za plastiki. Kila nambari ina sifa tofauti, matumizi, na athari zinazowezekana kwa afya. Hapa nimeandika muhtasari wa kina wa kila nambari ya resin na maana yake kiafya.
PLASTIKI ZENYE NAMBA 1 --> Kundi hili linajumuisha plastiki zenye PET (Polyethylene Terephthalate):
Zimetengenezwa na nini?
Plastiki za PET hupatikana kawaida katika chupa za maji, soda, na vifungashio.
Utumiaji: Inashauriwa kutumika mara moja tu kwani matumizi ya mara kwa mara yanaweza kusababisha kiwango cha kemikali za plastiki kuingia kwenye kinywaji unachotumia na huweza kuruhusu ukuaji wa bakteria.
Masuala ya Afya: Matumizi yasiyo sahihi ya aina hii ya plastiki husababisha kuvuja kwa kemikali aina ya trioxide ya antimoni na phthalates, ambazo zote zinaweza kusababisha hatari kwa afya.
chapisho: https://t.co/KoNF3DgzR7
chapisho: https://t.co/FBm5jCaKBp
Kundi la plastiki lenye alama namba 2 --> HDPE (High-Density Polyethylene):
Zimeundwa na nini?
Plastiki imara inayotumika katika makopo ya maziwa, vinyago, na vyombo vya sabuni nk.
Utumiaji: Inasifiwa katika tafiti kuwa salama na inaweza kuchakatwa tena.
Masuala ya Afya: Baadhi ya tafiti zinaonyesha uwezekano wa uvujaji wa kemikali aina nonylphenol, ambayo ina athari kwenye homoni, hasa kama hii plastiki itawekwa juani kwa muda mrefu.
PLASTIKI KUNDI ALAMA NAMBA 3 --> PVC (Polyvinyl Chloride):
Zimeundwaje?
Plastiki laini na rahisi kunyumbulika inayotumika kwenye vinyago, na sehemu za mabomba.
Utumiaji: Mara nyingi hujulikana kama "PLASTIKI ISIYO NZURI KIAFYA"; haishauriwi kwa kula au kunywa. Nchi nyingi zimeanza kuchukua tahadhari kuhusu aina hii ya plastiki.
Masuala ya Afya: Tafiti zinaonyesha Plastiki huweza kutoa kemikali aina phthalates, ambazo huharibu homoni, na athari kadhaa katika afya.
Moja ya Taarifa kutoka umoja wa Ulaya kuhusu matumizi ya bidhaa zenye PVC na afya
PLASTIKI ZENYE NAMBA 4 --> LDPE (Low-Density Polyethylene):
Zimeundwaje?
Hizi ni Plastiki ngumu, nyepesi na zisizoathiriwa na joto, mfano zinatumika katika mifuko ya mboga na kufunga chakula.
Utumiaji: Salama kiasi lakini haziwezi kuchakatwa tena.
Masuala ya Afya: Inaweza kutoa kemikali aina nonylphenol inayoathiri homoni, hasa ukiiweka juani. Usiiweke juani.
PASTIKI KUNDI NAMBA 5 -->PP (Polypropylene):
Zimeundwaje?
Hii ni Plastiki ngumu na nyepesi inayotumika katika vyombo vya maziwa ya mgando na vyombo vinavyotumika mara moja (Single use).
Utumiaji: Hii ni plastiki imara na inahimili joto.
Masuala ya Afya: Salama kiasi lakini inaweza kuwa inatoa plastiki ndogondogo (microplastics).
PLASTIKI KUNDI NAMBA 6 --> Polystyrene (PS):
Zimeundwaje?
Hutumika katika vikombe vinavyotumika mara moja, vyombo vya chakula, na vifungashio.
Utumiaji: Vigumu kuchakatwa tena.
Masuala ya Afya: Ikitumika zaidi ya mara moja huweza kutoa kemikali aina ya styrene japo athari za muda mrefu hazijawa wazi kuweza kufanya hitimisho.
chapisho: https://web.archive.org/web/20110824143749/http://plasticfoodservicefacts.com/main/Safety/Californias-Proposition-65/Q-A-on-the-Safety-of-Polystyrene-Foodservice-Products.GMEditor.html…
Kundi namba 7 ni plastiki nyingine (BPA, Polycarbonate, LEXAN).
HITIMISHO:
Nimekuandikia somo ili uelewe hata kwa kidogo kuhusu plastiki. Iwapo unatumia plastiki ni muhimu kufanya uchaguzi sahihi kuhusu utumiaji na utupaji wa bidhaa za plastiki. Wakati plastiki zingine zinachukuliwa kuwa salama kwa matumizi maalum, zingine zina hatari zinazowezekana kwa afya, na ni muhimu kutumia njia zetu za asili kuhifadhi vyakula ikiwemo vyombo vya udogo, chupa zisizo za plastiki nk.
Kwa muhtasari:
Kundi la plastiki lenye alama namba 1: ☑️Tumia ila usiirudie zaidi ya mara moja
Kundi la plastiki lenye alama namba 2: ☑️Ni salama kwa kiasi chake
Kundi la plastiki lenye alama namba 3: ❌ Punguza matumizi yake, jihakikishie haina phthalate
Kundi la plastiki lenye alama namba 4: ☑️Ni salama kwa kiasi chake
Kundi la plastiki lenye alama namba 5: ☑️Ni salama kwa kiasi chake
Kundi la plastiki lenye alama namba 6: ❌Kuna mashaka katika usalama wake
Kundi la plastiki lenye alama namba 7: ❌Kuna mashaka katika usalama wake
Upatapo elimu hii usisahau pia kushea kwa wale wote uwapendao ili nao wapate kujifunza.
Kujifunza zaidi kuhusu afya tembelea tovuti yangu: HOME | ISAYA FEBU
Ni mimi mwenye kujali afya yako Dr. Isaya Febu, nikutakie siku njema.