- Dr. ISAYA FEBU Newsletter
- Posts
- Dawa Muhimu Kwa Mama Mjamzito.
Dawa Muhimu Kwa Mama Mjamzito.
Dawa muhimu kwa mama mjamzito ni zile zinazosaidia afya ya mama na ukuaji mzuri wa mtoto tumboni.
Mara nyingi hizi siyo dawa za kutibu ugonjwa, bali ni virutubisho na kinga ambazo kila mama mjamzito anashauriwa kutumia kwa uangalizi wa daktari.

Leo katika mada yetu ya ukurasa huu tutazungumzia dawa muhimu kwa mama mjamzito. Ungana nami katika kuchambua dawa hizi.
1) Foliki Asidi (Folic Acid).
Hushauriwa kuanza kutumika hata kabla ya kushika mimba (kwa miezi 3 kabla ya kushika mimba) na miezi 3 ya mwanzo ya ujauzito (first trimester).
Husaidia kuzuia kasoro za neva kwa mtoto (neural tube defects) kama vile tatizo la mgongo wazi kwa mtoto (spina bifida).

Dozi ya kawaida: 400–800 mcg kwa siku.

2) Madini Ya Chuma (Ferrous Sulphate).
Huzuia na kutibu upungufu wa damu (anemia) unaosababisha uchovu na hatari wakati wa kujifungua.
Mara nyingi hutolewa pamoja na foliki asidi (FeFo).

3) Calcium.
Muhimu kwa mifupa na meno ya mtoto na mama.
Husaidia kuzuia shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito (pre-eclampsia).
4) Vitamin D.
Husaidia ufyonzaji wa calcium na ukuaji wa mifupa ya mtoto.
Pia huimarisha kinga ya mwili.
5) Multivitamins Kwa Wajawazito (Prenatal Vitamins).
Multivitamins zenye mchanganyiko wa vitamin na madini muhimu kama zinc, iodine, na vitamin B complex zinaongeza nguvu na kusaidia ukuaji wa mtoto tumboni.
6) Dawa Za Minyoo (Deworming).
Mara nyingi hutolewa baada ya trimester ya kwanza (miezi 3 ya mwanzo kupita).
Husaidia kuzuia upungufu wa damu unaosababishwa na minyoo. (Mfano: Mebendazole, Albendazole — hutolewa kwa ushauri wa daktari).
7) Chanjo ya tetenasi (Tetanus Toxoid Injection).
Kinga dhidi ya pepopunda (tetenasi) kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Angalizo:
Mama mjamzito hatakiwi kutumia dawa za kawaida (mfano antibiotics, dawa za maumivu, dawa za malaria) bila ushauri wa daktari, kwani baadhi zina madhara kwa mtoto tumboni.
Dawa zote lazima ziandikwe au kupendekezwa na daktari au mtaalamu wa afya.
HITIMISHO:
Dawa hizo hapo juu husaidia kuhakikisha afya njema ya mama na ukuaji mzuri wa mtoto tumboni.